Ushindi huo, umeifanya timu hiyo kutinga hatua ya 32 Bora ya michuano hiyo ambayo bingwa hucheza michuano ya CAF
Timu ya Azam FC, imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Alliance katika mfululizo wa mechi za michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC), mchezo uliopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Mabao ya Azam, yalifungwa na Allasane Diao na James Akaminko kipindi cha pili na kuifanya timu hiyo kusonga mbele.
Mchezo huo, ulikuwa na ushindani mkubwa na kufanya hadi dakika 45 za kwanza zikimalizika hakuna timu iliyoona lango la mwenzie.
Dakika 3 baada ya kuanza kwa kipindi cha pili, Diao alifunga bao la kwanza kwa Azam na dakika ya 56, Akaminko alifunga bao la pili kwa timu hiyo.
Katika dakika za nyongeza, mashabiki wa Azam wakiamini wameshinda 2-0, ndipo Eric Paul alipofunga bao la kufutia machozi kwa upande wa Alliance.
Ushindi huo, umeifanya Azam kutinga hatua ya 32 Bora ya michuano hiyo ambayo bingwa wake huiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.
Timu hiyo itashuka uwanjani Kaitaba Desemba 21 kuumana na Kagera Sugar.
Matokeo mengine;
Mbeya City 2-0 Lyon
Copco FC 1-2 Mabao FC
Ruvu Shooting 0-1 Mkwajuni FC
TMA FC 7-2 Sharp Lion
KMC FC 4-2 ACA Eagle