Azam FC yarejea kileleni Ligi Kuu

© Kwa Hisani

KANDANDA Azam FC yarejea kileleni Ligi Kuu

Zahoro Mlanzi • 18:34 - 04.11.2023

Azam sasa wakifikisha alama 19 wakiwa wameshuka dimbani mara nane wakiwaacha Yanga na Simba ambao wanacheza kesho wakiwa na alama 18.

Kiungo wa timu ya Azam FC, Sospeter Bajana, amefunga mabao mawili na kuisaidia timu yake kuibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya Ihefu FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Highland Estate, Mbeya.

Kwa matokeo hayo, Azam sasa wanakwea kileleni wakifikisha alama 19 wakiwa wameshuka dimbani mara nane wakiwaacha Yanga na Simba ambao wanacheza kesho wakiwa na alama 18.

Mchezo huo ulitabiriwa kuwa mgumu hasa kutokana na hali ya mvua zinazoendelea katika mikoa mbalimbali ya Tanzania na kuleta hofu kubwa ikuhusu hali ya uwanja.

Hata hivyo, mechi hiyo ilianza kwa uzuri na timu zote kujenga mashambulizi yao ya kutafuta bao la utangulizi.

Azam wamefunga bao la kwanza kupitia kwa Feisal Salum 'Fei Toto' dakika ya 34 kwa kichwa akiunganisha mpira wa kona wa Kipre Junior. Bao hilo lilidumu hadi timu hizo zinakwenda mapumziko.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Azam walirejea tena kambani mapema kabisa dakika ya 46 likifungwa na Bajana.

Bajana tena alikamilisha ushindi huo kwa kufunga bao la tatu dakika ya 48 na kushusha presha kwa Kocha Youssouph Dabo. Bao la kufutia machozi la Ihefu lilifungwa dakika ya 90 na mshambuliaji, Jaffar Kibaya ambaye aliingia akitoka benchi.

Ushindi huo ni wa pili mfululizo kwa Azam baada ya kutoka kupoteza katika michezo miwili mfululizo.