Ni baada ya kutoka 0-0 na Tabora United katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi
Timu ya Azam FC, imepanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kutoka suluhu na Tabora United kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mkoani hapa.
Azam iliingia kwenye mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 4-0 waliopata kwa mara ya kwanza timu hizo zilipokutana kwenye ligi Agosti, mwaka jana.
Hata hivyo safari hii vijana wa Tabora United walionekana kuwa katika wakati mzuri na wangeweza kupata mabao kama Emotan Cletus na Jackson Mbombo wangeweza kutumia vizuri nafasi zilizotengenezwa kwa upande wa timu yao.
Hii ni sare ya pili kwa Azam katika mechi tatu walizocheza tangu kurejea kwa ligi hiyo. Kabla ya ligi kusimama Azam walikuwa na mfululizo wa kupata ushindi katika mechi sita.
Kwa matokeo hayo, Azam imefikisha alama 36 ambazo zimewapandisha hadi nafasi ya pili ambazo ni sawa na Simba waliopo kwenye nafasi ya tatu na wakiwa na mechi moja mkononi ila zinatofautiana kwa mabao.
Mara baada ya mchezo huo, Azam italazimika kusafiri hadi Mbeya kwa ajili ya mchezo dhidi ya Tanzania Prisons, Februari 25.
Katika mechi nyingine, iliyochezwa leo, timu ya Ihefu FC, imeendeleza umwamba wake kwa kuibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Geita Gold ambao walikuwa wenyeji wa mchezo huo.
Wachezaji wapya waliosajiliwa na kikosi hicho cha Ihefu wakati wa usajili wa dirisha dogo, Marouf Tchakei na Elvis Rupia kila mmoja alifunga bao moja katika dakika 13 za kwanza.
Hiyo inakuwa ni mara ya pili wachezaji hao kufunga ikiwa pia walifanya hivyo katika mechi iliyopita ambapo waliibuka na ushindi wa 3-2 dhidi ya Mtibwa Sugar.
Bao la kufutia macho kwa upande wa Geita Gold lilifungwa kipindi cha pili na Tariq Seif. Geita tangu kurejea kwa ligi wamepoteza mechi ya tatu mfululizo huku Ihefu wao wakishinda mechi yao ya pili mfululizo.