Azam FC yatamba kutembeza kichapo kwa kila timu

KANDANDA Azam FC yatamba kutembeza kichapo kwa kila timu

Na Zahoro Mlanzi • 15:44 - 15.11.2023

Timu hiyo imerejea mazoezini wiki iliyopita baada ya kucheza mechi zao mbili za ugenini na kuondoka na alama zote sita

Matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, timu ya Azam FC, imetamba itaendelea na kasi waliyoishia nayo hususani katika mechi za ugenini za Ligi Kuu Bara ili kuendelea kubaki juu katika msimamo wa ligi hiyo.

Timu hiyo ilirejea mazoezini wiki iliyopita baada ya kucheza mechi zao mbili za ugenini na kuondoka na alama zote sita dhidi ya Ihefu FC ya Mbeya na Mashujaa FC ya Kigoma.

Katika mechi hizo, Azam ilianza kwa kuitandika Mashujaa mabao 3-0 uwanjani Lake Tanganyika kabla ya kuifunga Ihefu mabao 3-1 uwanjani Highland Estate.

Matokeo hayo, yameifanya Azam FC kubaki katika nafasi ya pili ikiwa na alama 19 sawa na Simba SC huku Yanga ikiongoza ikiwa na alama 24.

Akizungumzia maandalizi yao kwa ujumla, Ofisa Habari wa timu hiyo, Hasheem Ibwe, amesema bado hawajapoa wanahitaji kuendelea na kasi hiyo kwenye mechi zote.

“Bado tupo vizuri na benchi la ufundi linawapa mbinu wachezaji wetu kwa ajili ya mechi zotekuona kwamba tunapata ushindi hivyo tutazidi kupambana zaidi kwa ajili ya kupata pointi tatu," amesema Ibwe na kuongeza.

“Ushindani ni mkubwa hilo tunalitambua na sisi tutaendelea kuleta ushindani kwa kuwa tunatimu bora yenye wachezaji ambao wanaleta ushindani, mashabiki wazidi kuwa pamoja na sisi”.

Hata hivyo, wakati timu hiyo ikiendelea na maandalizi yao, nyota wake sita wameitwa katika timu mbalimbali za Taifa ambazo zinajiandaa na mechi za kufuzu Kombe la Dunia.

Nyota hao ni Lusajo Mwaikenda, Feisal Salum 'Fei Toto', Abdul Seleman 'Sopu', Edward Manyama na Sospeter Bajana wameitwa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' huku Prince Dube akienda kuichezea Zimbabwe.

Tags: