Aziz Ki kujiunga na Yanga juu kwa juu Kigali

KANDANDA Aziz Ki kujiunga na Yanga juu kwa juu Kigali

Zahoro Mlanzi • 17:05 - 12.09.2023

Aziz Ki bado yupo katika majukumu ya timu yake ya Taifa ambayo kesho itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Morocco.

Klabu ya Yanga SC, imeweka wazi kiungo wake mshambuliaji raia wa Burkina Faso, Stephano Aziz Ki, atajiunga na wenzake pindi timu hiyo itakapotua nchini Rwanda.

Aziz Ki bado yupo katika majukumu ya timu yake ya Taifa ambayo kesho itacheza mechi ya kirafiki nchini Ufaransa dhidi ya Morocco.

Kiungo huyo pamoja na timu yake ya Burkina Faso, walizua taharuki baada ya kutokea Tetemeko la Ardhi nchini Morocco lililosababisha vifo vya zaidi ya watu 2,500 wakiwa nchini humo, lakini wao walisalimika.

Akizungumza na Pulsesports, Ofisa Habari wa timu ya Yanga, Ally Kamwe, amesema kwa ratiba ilivyo ni ngumu Aziz Ki kuwahi kurudi Tanzania na kisha aende Rwanda.

"Azizi Ki kwa sasa yupo jijini Paris na timu yake ya Taifa wakisubiri kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Morocco, watakapomaliza moja kwa moja atatafuta ndege ya kumleta Kigali, Rwanda," amesema Kamwe.

"Hawezi kutuwahi hapa Tanzania, hivyo siku ambayo tutafika sisi jijini Kigali ambayo ni Ijumaa, ni matumaini yetu na yeye atatukuta Kigali tukimsubiri ajiunge na wenzake kuelekea mchezo wetu wa Jumamosi," ameongeza.

Akizungumzia maandalizi kwa ujumla kuhusu mchezo huo dhidi ya Al-Merreikh utakaopigwa Uwanja wa Pele jijini Kigali, Kamwe amesema timu inaendelea na mazoezi ya mwisho mwisho na ina morali kubwa kuelekea mchezo huo.

Amesema hadi sasa tayari zaidi ya mabao 37 yamethibisha kuambatana na timu hiyo kwenda kutoa sapoti jijini Kigali.

"Tuna imani tutafikisha mabasi 50, itakuwa ni historia kwa soka la Afrika, kila kitu tumeweka sawa kuhusu jinsi watakavyoingia na kiingilio cha chini kwa fedha ya Tanzania ni sh. 15,000, hivyo kila kitu kinakwenda vizuri," amesema

Tags: