Hiyo ni katika kufanya hamasa ili timu hiyo iweze kuibuka na ushindi katika mechi yao inayofuata ya kimataifa itakayopigwa Jumatano
Mfadhili wa Klabu ya soka ya Yanga, Ghalib Said Mohamed 'GSM', ametoa sh. milioni 225 za Kitanzania kwa ajili ya kununua tiketi zipatazo 45,000 za viti vya jukwaa la mzunguko ili mashabiki wajitokeze uwanjani kwenda kuwapa hamasa wachezaji wakati wa mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Medeama SC.
Mchezo huo ambao ni muhimu kwa Yanga ni wa mzunguko wa nne kwa timu zote na unatarajia kuchezwa Jumatano kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, amesema uongozi wa timu hiyo umeuchukulia mchezo huo kwa upekee wa aina yake na ndio maana hatua mbalimbali za kutaka kuhakikisha ushindi unapatikana zimekuwa zikifanyika.
"Huu ni mchezo wetu muhimu zaidi lakini pia bila kusahau utakuwa ni mchezo mgumu, hivyo kwa kuona hivyo tumeona kuongeza nguvu ya mashabiki ambapo GSM amenunua tiketi zote za mzunguko ili watu wajitokeze kwa uwingi," amesema.
Yanga wanashika mkia katika Kundi D nyuma ya Al Ahly, CR Belouizdad na Medeama. Hata hivyo nafasi bado ipo wazi kwa kila timu kusonga mbele na kama Yanga watawafunga Medeama katika mchezo huo watakuwa wamejiweka sehemu nzuri zaidi.
Timu hizo zilikutana wiki mbili zilizopita katika mchezo uliofanyika Ghana na zilitoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1.
Katika hatua nyingine, kiwango cha upachikaji mabao kwa kiungo wa Yanga, Stephan Aziz KI, kimemuibua kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi ambapo amesema alimtuma kazi hiyo kabla ya kuanza kwa msimu.
Akizungumza mara baada ya mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar ambapo Yanga walishinda mabao 4-1 huku Aziz Ki akifunga mabao mawili, Gamondi, amesema baada ya kumuona tu kiungo huyo aliongea naye na kumwambia kuwa anataka mchezaji huyo awe Mfungaji Bora.
"Nilipokuwa katika maandalizi ya msimu niliona uwezo wa Aziz na hapo ndio nikamwambia kuwa nataka wewe uwe mfungaji bora wete na ligi," amesema.
Azizi Ki kwasasa yupo katika kiwango kizuri cha upachikaji mabao akiwa ni kinara kwenye ligi hiyo kwa mabao yake 9 ndani ya mechi 10 alizocheza.
Idadi hiyo ya mabao 9 ndiyo aliyofunga katika msimu mzima uliopita.