Kipa huyo wa Yanga ametwaa tuzo hiyo akiwazidi wachezaji wenzake, Ibrahim Abdullah na Kouassi Yao
Kipa Djigui Diara, amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa timu ya Yanga SC wa mwezi Desemba.
Tuzo hiyo inatolewa na Shirika la Bima ya taifa (NIC) na Diara anakuwa ni mchezaji wa tatu kushinda baada ya Stephan Aziz Ki na Pacome Zouzoua kutangulia katika miezi miwili iliyopita.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na klabu hiyo, Diara ameshinda tuzo hiyo kwa kuwashinda wachezaji wenzie, Ibrahim Abdullah 'Bacca' na Kouassi Yao ambao aliingia nao tatu bora.
Katika mwezi uliopita, Diara alicheza mechi tatu za Ligi ya Mabingwa Afrika na mbili za Ligi Kuu Bara na aliruhusu mabao matatu kwenye mechi zote hizo.
Kwasasa, kipa huyo yupo na kikosi cha timu ya Taifa ya Mali akijiandaa na michuano ya Afcon ambayo inatarajiwa kuanza wiki Ijayo.
Mali katika fainali za michuano hiyo ambayo zitafanyikia nchini Ivory Coast, ipo kundi moja na Namibia, Afrika Kusini na Tunisia.