Nyota huyo amekuwa na kiwango bora katika miezi miwili ya hivi karibuni hadi kujumuishwa katika kikosi cha Taifa Stars
Kiungo wa klabu ya soka ya Azam FC, Feisal Salum 'Fei Toto', ameshinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Tanzania kwa mwezi Novemba akiwazidi kete mchezaji mwenzie, Kipre Junior na wa Yanga, Max Nzengeli.
Katika mwezi huo, Fei Toto, amecheza dakika 270 sawa na mechi tatu ambapo amefunga mabao mawili na kutoa pasi nne za mabao kwa wenzie.
Fei amekuwa katika kiwango bora hasa mwezi uliopita na hiyo ilisababisha hadi Kocha wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Adel Amrouche kumrudisha katika timu hiyo baada ya kumuacha katika vikosi kadhaa.
Kiwango ambacho anaonesha kwa mechi za hivi karibuni kimefanya kuwakumbusha mchezaji huyo enzi hizo akiwa na timu yake ya zamani ya Yanga, ambayo alikuwa akicheza kabla ya kuhama mwisho wa msimu uliopita.
Mbali na Feisal lakini pia Kocha Mkuu wa kikosi cha Azam, Bruno Ferry, ameshinda tuzo ya Kocha Bora kwa mwezi huo baada ya kuingoza timu yake kushinda michezo mitatu ambayo ni dhidi ya Mashujaa FC, Ihefu FC na Mtibwa Sugar.
Ferry amewashinda kocha wa Yanga, Miguel Gamondi na Kocha wa Singida FG, Heron Ricardo.