FIFA yaipiga 'stop' Simba SC kusajili

KANDANDA FIFA yaipiga 'stop' Simba SC kusajili

Na Zahoro Mlanzi • 17:00 - 23.11.2023

Uamuzi huo umefanywa baada ya klabu hiyo kushinda kesi ya madai dhidi ya Simba kutokana na mauzo ya Pape Ousmane Sakho

Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), limeifungia Klabu ya Simba ya Tanzania kufanya usajili hadi watakapoilipa Klabu ya Teungueth ya Senegal iliyowauzia winga, Pape Ousmane Sakho.

Uamuzi huo umefanywa baada ya klabu hiyo kushinda kesi ya madai dhidi ya Simba kutokana na mauzo ya Sakho ambaye mwishoni mwa msimu uliopita alijiunga na klabu ya Quevilly Rouen Metropole ya Ufaransa.

Kutokana na adhabu hiyo, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) nao wameifungia Simba kufanya usajili wa ndani ambapo dirisha lake linatarajiwa kufunguliwa Desemba 15.

Katika hatua nyingine, timu ya Simba, imeendelea na kambi yao ya maandalizi kuelekea mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo watacheza Jumamosi dhidi ya Asec Mimosa ya Ivory Coast.

Mchezo huo unatarajia kufanyika katika Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni kwa saa za Afrika Mashariki na Kati.

Baadhi ya wachezaji ambao walikuwa katika majukumu ya timu za Taifa kama Henock Inonga na Cloutas Chama sambamba na wale waliokuwa na timu ya Taifa ya Tanzania, wote wapo kambini wakiendelea na mazoezi chini ya Kocha, Daniel Cadena.

Wakati huohuo, Klabu ya Asec Mimosa, imewasili nchini tangu Jumatano alfajiri.

Asec wametua na msafara wa wachezaji na viongozi jumla yao ikiwa ni 31 kama ilivyoelezwa hapo awali na walionekana wakiwa hawana wasiwasi wowote.

Tags: