Kauli hiyo ameitoa kocha huyo wa Yanga wakati wakijiandaa kuumana na KMC Jumamosi
Kocha wa timu ya Yanga SC, Miguel Gamondi, amesema licha ya kumaliza mzunguko wa kwanza wakiwa kileleni lakini bado anajua kuna kazi kubwa ya kufanya wakati huu duru la pili linapoanza.
Hayo amesema wakati akifanya maandalizi na kikosi chake ya kukabiliana na KMC katika mchezo wa kwanza mzunguko wa pili unaotarajia kuchezwa Jumamosi Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
"Tunaelekea kuanza mzunguko wa pili na tunatarajia ugumu zaidi tofauti na ilivyokuwa mzunguko wa kwanza, hivyo ili kuchukuwa ubingwa bado tunakabiliwa na kazi kubwa mbele yetu," amesema.
Kuelekea mchezo wa KMC, Kocha Gamondi amesema anakumbuka waliwafunga mabao 5-0 katika mchezo wa kwanza lakini huu ni mchezo mwingine na timu hiyo imebadilika.
Amesema amewaona katika baadhi ya michezo kadhaa ya ligi waliyocheza na anaamini kuwa mchezo utakuwa mgumu.
Katika hatua nyingine, Gamondi amewasifu mashabiki kwa Yanga kwakuwa siku zote wamekuwa nyuma ya timu yao Kila inapokwenda uwanjani.
"Mashabiki wetu ni moja kati ya silaha muhimu sana kwakuwa wapo na sisi katika nyakati zote na kila sehemu," amesema.