CAF hawajateua waamuzi kutoka Tanzania kwa AFCON 2023 licha ya kuwa na Ligi Bora. Viongozi wa Tanzania wachukulia kama changamoto.
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), limetoa orodha ya waamuzi 32 wa kati na wasaidizi wake 33 kwa ajili ya michuano ya AFCON 2023 itakayofanyika mwakani nchini Ivory Coast.
Katika orodha hiyo, Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), imetoa waamuzi wanne kutoka Kenya iliyotoa wawili, Sudan na Djibouti.
Waamuzi hao ni Peter Kamaku wa Kenya akiwa mwamuzi wa kati, Ibrahim Mohamed wa Sudan, Liban Abdoulrazack wa Djibouti na Yiembe Stephen wa Kenya wakiwa waamuzi wasaidizi.
Gumzo limekuja baada ya Tanzania kuwa ni miongoni mwa mataifa matano yenye Ligi Bora Afrika, sasa inawezekanaje ikashindwa kutoa mwamuzi kuchezesha michuano hiyo.
Katika kutoa ufafanuzi wa hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi nchini, Nassor Hamduni, amesema hiyo ni changamoto ambayo inapaswa kufanyiwa kazi ili michuano ijayo waweze kuwa na wawakilishi.
"Ninachoweza kusema tumekosa bahati si kitu cha ajabu kukosa nafasi kwani wataendelea kujipanga ili waweze kupata nafasi wakati ujao," amesema Hamduni.
Amesema wadau wengi wa soka wanasuburi hadi wakosee ndipo wanajitokeza kukosoa kitu ambacho si kizuri kwani si Tanzania pekee iliyokosa yapo mataifa mengi Afrika.
"Mbona hamjapongeza alipokwenda Arajiga (Ahmed) kuchezesha AFCON ya vijana, lakini limetokea hili tunaanza kumtafuta mchawi," amesisitiza.
Pia Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almas Kasongo, amesema suala hilo linatakiwa kupokelewa vizuri na kulifanyia kazi na si kuanza kulaumiana.
"Kwangu ni changamoto na tunatakiwa kuipokea kwa uzuri wake na kuigeuza kuwa jambo lenye manufaa kwetu, mambo ya uteuzi yanakuwa na vigezo vyake," amesema Kasongo na kuongeza.
"Sitaki kuamini kama wamekosea au kupendelea watu fulani, walifanya uamuzi kutokana na vigezo walivyojiwekea wenyewe, sisi kwetu itabaki kama changamoto."
Tanzania imefuzu kucheza fainali zake za tatu za AFCON mwaka huu ikimaliza ya pili nyuma ya Algeria.