Idadi ya mechi Uwanja wa Taifa kupunguzwa

KANDANDA Idadi ya mechi Uwanja wa Taifa kupunguzwa

Zahoro Mlanzi • 20:28 - 27.11.2023

Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia ili kuulinda uwanja huo

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallec Karia, amesema wanafikiria kupunguza matumizi katika Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.

Karia ametoa kauli hiyo wakati alipofanyiwa mahojiano maalum na Cloud's TV ya jijini Dar es Salaam.

Amesema uwanja huo ni moja kati ya viwanja bora Afrika na ndio maana kumekuwa na maombi mengi ya timu kutoka nje kutaka kuutumia hivyo ni vyema kuulinda.

Karia amesema wanafikiria kupunguza idadi ya mechi hasa za Ligi Kuu kuchezwa katika uwanja huo na badala yake mechi ambazo zitakuwa na uzito mkubwa kama vile michuano ya kimataifa au mechi kati ya Yanga na Simba ndio ziendelee kufanyika hapo.

"Uwanja wetu ni mzuri na hivyo tunapaswa kuutumia vizuri, najua hii ni mali ya serikali lakini sisi kama wadau wa soka lazima tushiriki katika kuutunza maana ukiwa mbovu ni hasara kwetu sote," amesema.

Karia amesema hata kwa upande wa timu ya Taifa wataangalia namna ya kutafuta sehemu ya kuzicheza mechi zao hivyo na klabu zinazopendelea kuutumia uwanja huo ziwe na viwanja mbadala.

Uwanja huo ambao ni mali ya serikali umetoka kufanyiwa ukarabati mkubwa hivi karibuni na ulikuwa ni mwenyeji wa ufunguzi wa michuano ya AFL ambapo Simba walikuwa wenyeji wa Al Ahly ya Misri.

Baada ya kufunguliwa zimeshafanyika mechi kadhaa ikiwemo ya Simba na Yanga lakini pia mechi za kimataifa ambapo Simba waliwakaribisha Asec Mimosa, hivi karibuni ilichezwa mechi kati ya timu ya Taifa 'Taifa Stars' dhidi ya Morocco.

Tags: