JKT Queens yaahidi makubwa Ligi ya Mabingwa Afrika

© Active Media

KANDANDA JKT Queens yaahidi makubwa Ligi ya Mabingwa Afrika

Zahoro Mlanzi • 21:00 - 12.10.2023

JKT ipo Kundi A pamoja na mwenyeji, Athletico FC ya Ivory Coast, Sporting Casablanca ya Morocco na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Timu ya JKT Queens, imetamba kufanya vizuri katika kundi lao licha ya kupangwa na timu ngumu katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake 2024.

JKT ipo Kundi A pamoja na mwenyeji, Athletico FC ya Ivory Coast, Sporting Casablanca ya Morocco na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Kundi B linaundwa na mabingwa watetezi, AS FAR ya Morocco, Ampem Darkoa ya Ghana, Huracanes FC ya Guinea ya Ikweta na AS Mande ya Mali.

Michuano hiyo itaanza Novemba 5 hadi 19 kwa mechi kupigwa katika viwanja vya Laurent Pokou jijini San Pedro na Amadou Gon Coulibaly jijini Korhogo, Ivory Coast.

Ofisa Habari wa timu hiyo, Masau Bwire, amezungumzia mipango yao kwa kuwatoa hofu Watanzania kuwa watajiandaa vizuri kuhakikisha wanafanya vizuri katika michuano hiyo.

"Wengine walisema kundi hilo ni gumu kutokana na wapinzani tuliopangwa nao, wanaona ni mzigo mkubwa kwetu, niwaambie labda hawana historia nzuri ya Soka la Wanawake Tanzania...Afrika wanaiogopa Tanzania katika ubora wa soka hilo, ndio maana JKT ni mabingwa wa Tanzania na ndio mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati," ametamba Bwire.

Amesema pamoja na Atletico kuwa mwenyeji wa mashindano hayo kutokana na kutwaa ubingwa mara mbili mfululizo nyumbani kwao, hawana hofu nao kwani ni wageni katika mashindano hayo.

Amesema Wamoroco pia ni wageni wao ni mara ya kwanza kushiriki, hivyo hawaoni shaka juu ya uzito wao kwani watapambana.

Kwa upande wa Mamelod, amesema wao wameshiriki kila mwaka na ndio mabingwa wa kwanza wa michuano hiyo ilipoanzishwa.

"Tutakwenda kufanya makubwa...vigumu vyote hulainishwa, kwani lengo letu ni kucheza fainali ya michuano hii," amesisitiza Bwire.

Tags: