Kocha Azam aisifia Yanga SC, aahidi kupambana nao

Ligi Kuu: Kocha Azam aisifia Yanga SC, aahidi kupambana nao

Na Zahoro Mlanzi • 18:00 - 22.10.2023

Amewaomba mashabiki wao kujitokeza kwa wingi.

Kocha Msaidizi wa timu ya Azam FC, Bruno Ferry, amesema wanajua Yanga SC ni timu kubwa nchini Tanzania lakini watapambana kuhakikisha wanaondoka na alama tatu.

Yanga itaikaribisha Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaopigwa kesho kuanzia saa 12. 30 uwanjani Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.

Timu hizo zinashuka uwanjani huku Yanga ikiwa nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo kwa alama 12 na Azam ikishika nafasi ya pili ikiwa na alama 13 nyuma ya Simba yenye alama 15.

Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuelekea mchezo huo, Ferry amesema hajui nini kitatokea lakini wana matumaini mchezo utakuwa mzuri.

"Ni mchezo mkubwa kwa Tanzania na tunakutana na timu kubwa ya Yanga, huo ni mchezo maalum kwetu kuonesha ubora wa kikosi chetu, tupo tayari kupambana kupata matokeo mazuri ya alama tatu," amesema Ferry.

Ameongeza huo ni mchezo tofauti na ule wa Ngao ya Jamii ambao walifungwa 2-0 na Yanga na kwamba wamejipanga kuhakikisha wanaondoka na ushindi hivyo mashabiki wao wajitokeze kwa wingi siku hiyo.

Kwa upande wa Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema wamekuwa na wiki ngumu kutokana na nyota wao 10 kuitwa katika timu za taifa hivyo maandalizi yamefanyika kutokana na wachezaji waliokuwepo.

"Ukiangalia Azizi KI (Stephen) amechelewa kurudi, amerudi Ijumaa hivyo hajapata hata muda wa kupumzika vizuri anatakiwa kumtumia tena, kwa ujumla muda umekuwa mdogo lakini tutahakikisha tunapata matokeo mazuri," amesema Gamondi.

Amesema watashambulia mwanzo mwisho huku wakizuia kwa umakini kwani ili kushinda mechi unatakiwa kucheza hivyo.

Amewaomba mashabiki wao kujitokeza kwa wingi akiamini shabiki ni mchezaji wa 12 uwanjani, hivyo wataongeza hamasa kwa wachezaji wao kujituma zaidi.

Tags: