Kocha Stars: Tupo tayari kwa AFCON

KANDANDA Kocha Stars: Tupo tayari kwa AFCON

Na Zahoro Mlanzi • 21:00 - 12.01.2024

Timu hiyo itashuka uwanjani Januari 17 kuumana na Morocco katika mchezo wa kwanza wa Kundi D

Kocha Msaidizi wa timu ya Taifa 'Taifa Stars', Hemed Seleman 'Morocco', amesema kwa sasa kikosi chao kipo tayari kwa ajili ya michuano ya AFCON kutokana na maandalizi waliyofanya.

Timu hiyo ambayo kwa sasa imekita kambi katika Mji wa San Pedro, Ivory Coast, imecheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Morocco na Misri.

Stars ambayo inashiriki fainali hizo kwa mara ya tatu katika historia yake, imepangwa Kundi D pamoja na timu za Morocco, DR Congo na Zambia ambapo Stars itaanza kuumana na Morocco.

Akizungumza wakati wa mazoezi yaliyofanyika uwanjani Stade Auguste Denis Est, Seleman amesema makosa yaliyojitokeza katika mechi mbili za kirafiki wameshayafanyia kazi na sasa wapo tayari kwa mashindano.

"Kabla ya kufika hapa tumecheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Morocco na Misri, wachezaji wameonekana kufuata maelekezo yetu kwa kiasi kikubwa kitu kinachotufanya tuamini kuwa tupo tayari sasa kwa mashindano," amesema kocha huyo.

Amewaomba Watanzania kwa ujumla kuendelea kuiombea timu hiyo ifanye vizuri katika mechi zao zote za hatua ya makundi.

Kwa upande wa beki wa timu hiyo ambaye pia anaichezea Yanga SC, Dickson Job akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, amesema kama wachezaji wapo tayari kwa ajili ya mapambano kwani ushindani wa mazoezini umedhihirisha hilo.

"Tunajua tupo katika kundi gumu kutokana na timu zingine kuwa na wachezaji nyota ila sisi tunajivunia vipaji na jinsi tutakavyojituma uwanjani ndio itatupa matokeo chanya," amesema Job.

Amesema timu ya Morocco wameshacheza nao na yale makosa waliyofanya dhidi yao kama wachezaji kutokana na maelekezo ya makocha wao wameyafanyia kazi ipasavyo.

Ameongeza mchezo wa kwanza ndio utakaotoa taswira ya hatma yao katika kufanya vizuri kwenye michuano hiyo.

Tags: