Robertinho amuita Chama haraka kambini

KANDANDA Robertinho amuita Chama haraka kambini

Zahoro Mlanzi • 19:00 - 11.09.2023

Robertinho amesema anahitaji kuwa na umoja na mshikamano wakati wakianza safari yao kwenda Zambia na si kukutana juu kwa juu.

Kocha wa timu ya Simba, Robertinho Oliviera, amesema anataka nyota wote wa timu hiyo kuwahi kambini na kuondoka kwa pamoja katika safari yao ya kwenda Zambia.

Kauli hiyo imekuja baada ya kuelezwa kiungo wake, Mzambia Clatous Chama, ameomba kubakia nchini humo akiwasubiri akijiandaa na mchezo wao dhidi ya Power Dynamos ya nchini humo.

Mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika unatarajiwa kuchezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa mjini Ndola.

Akizungumza wakati wa mazoezi ya timu hiyo, Robertinho amesema anahitaji kuwa na umoja na mshikamano wakati wakianza safari yao kwenda Zambia na si kukutana juu kwa juu.

"Niliambiwa Chama anatusubiri Zambia kwakuwa tutakwenda kucheza huko ila nimewaambia viongozi kama amemaliza majukumu ya timu yake ya taifa anatakiwa kurudi kambini kufanya maandalizi ya pamoja na wenzake," amesema Robertinho.

Amesema mipango yake ni kuhakikisha wanashinda mechi hiyo ya ugenini ili kujiweka katika mazingira mazuri ya mchezo wa marudiano.

Ameongeza wakiwa kambini katika wiki ya mwisho ya maandalizi inakuwa rahisi kama kutakuwa na mfumo wa kuongezea kuushika kwa pamoja na si kila mtu kumuelekeza kwa muda wake.

Katika hatua nyingine, beki kisiki wa timu hiyo, Mkongo Henock Inonga, kesho anatarajia kujiunga na wenzake kujiandaa na mchezo huo akitoka kulitumikia taifa lake la DR Congo.