Simba SC kufyeka nyota 5 dirisha dogo

Kiungo wa Simba SC, Nassor kapamba ambaye anatajwa atatemwa ndani ya timu hiyo

KANDANDA Simba SC kufyeka nyota 5 dirisha dogo

Na Zahoro Mlanzi • 19:07 - 10.01.2024

Nyota hao ni wale walioshindwa kufanya vizuri ndani ya Klabu hiyo tangu wasajiliwe na pia walipewa nafasi ya kucheza Mapinduzi Cup

Zikiwa zimebaki siku tano kabla ya dirisha la usajili kufungwa Tanzania Bara, uongozi wa Klabu ya Simba, umepanga kuwatema wachezaji zaidi ya watano.

Wachezaji hao ni wale ambao wameshindwa kuonesha makali yao katika kikosi cha kwanza tangu wasajiliwe au waliopandishwa kutoka katika timu ya vijana.

Baadhi ya nyota ambao wanatajwa kupitiwa na panga hilo ni pamoja na Nassor Kapama, Shaban Chilunda, Jimyson Mwanuke, Ahmed Feruz na Abdallah Khamis ambao wote ni wazawa.

Mbali na wachezaji hao lakini pia wapo wachezaji wa kimataifa ambao wanaweza wakaunganishwa kwenye panga hilo ili kupisha nafasi za wachezaji wapya ambao wamesajiliwa akiwemo Babacar Sarr.

Asilimia kubwa ya wachezaji ambao wanatarajia kuachwa walikuwepo wapo visiwani Zanzibar kushiriki michuano ya Mapinduzi Cup isipokuwa Kapama ambaye kabla ya michuano hiyo alikuwa amefungiwa kwa kosa la utovu wa nidhamu.

Chilunda na Abdallah walijiunga na Simba mwanzoni mwa msimu huu lakini wameshindwa kutoboa kwenye kikosi cha kwanza na hivyo nafasi zao zinatakiwa kuwa wazi ili kupisha maingizo mapya.

Aidha kipa ambaye amedumu kikosini hapo kwa muda mrefu tangu timu za vijana, Feruz huenda akatolewa kwa mkopo ama kuachwa moja kwa moja kwasababu nafasi yake kikosini inaonekana kuwa finyu kutokana na makipa waliopo mbele yake.

Akizungumza na Pulsesports, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema hana taarifa rasmi kuhusu wachezaji wanaoachwa lakini alikiri kuwa katika dirisha la usajili lolote linaweza kutokea.

"Kwasasa sina taarifa kama kuna mchezaji ambaye anaachwa lakini katika dirisha la usajili jambo hilo ni kawaida, kama sisi tunavyosajili kutoka timu nyingine basi na timu nyingine zinachukuwa wachezaji kwetu," amesema.

Simba katika dirisha hili wamefanya usajili wa wachezaji wawili hadi sasa wakimuongeza kikosini Saleh Karabaka ambaye ametoka timu ya JKU pamoja na Msenegal, Sarr.

Tags: