Huyo anakuwa ni mchezaji wa tatu kusajiliwa na timu hiyo chini ya kocha, Abdelhak Benchikha katika dirisha dogo la usajili litakalofungwa leo saa 6 usiku
Klabu ya Simba, imemtambulisha straika wa kimataifa wa Gambia, Pa Omar Jobe, 25, kuja kuongeza nguvu ndani ya timu hiyo.
Utambulisho huo umekuja siku moja baada ya Kocha Mkuu, Abdel Benchika kuweka wazi kuwa anahitaji straika mpya ndani ya kikosi chake.
Kusajiliwa kwa straika huyo, ni wazi mastraika wa kigeni waliopo Jean Baleke au Mosses Phiri, mmojawapo atalazimika kumpisha Jobe kuanza maisha mapya ndani ya timu hiyo.
Huyo anakuwa mchezaji wa tatu kusajili kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo baada ya Salehe Karabaka wa JKU na Babacar Sarr wa Senegal.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mtandao wa kijamii wa klabu hiyo, straika huyo ameingia mkataba wa miaka miwili kuhudumu ndani ya kikosi hicho cha Msimbazi.
Taarifa zaidi kutoka vyanzo mbalimbali vya habari Afrika, zimeeleza kuwa Jobe timu yake ya mwisho kucheza ni Zheniz ya nchini Kazakhstan.
Jobe amejiunga na Zheniz mwaka jana akicheza michezo 16 na kufunga bao 1 huku pia katika msimu wa 2022/23 alihudumu ndani ya kikosi cha Neman Grodno ambapo alifunga bao 1 pia katika mechi 15.
Katika maisha yake ya soka, straika huyo, alifunga mabao matatu 'hat trick' yake ya kwanza mwaka 2021 akiwa na timu ya Sheikh Jamal Dhanmondi ya Ligi Kuu ya Bangladesh katika mchezo dhidi ya Arambagh ambapo katika mchezo huo alifunga mabao manne.
Baada ya kuwa na misimu mizuri ndani ya Bangladesh, Jobe alijiunga na KF Shkendija ya Macedonia akiwa mchezaji huru lakini alishindwa kuingia katika kikosi cha kwanza na kutolewa kwa mkopo kwenda Struga ya nchini humo kumalizia msimu.