Mechi hizo zinatarajiwa kuchezwa Jumanne na Jumatano baada ya mapumziko ya zaidi ya mwezi mmoja
Klabu za Simba na Yanga, zinatarajia kushuka uwanjani mwisho wa mwezi huu kwa ajili ya kucheza mechi zao za michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) za raundi ya pili.
Mechi za raundi ya pili ya michuano hiyo zilichezwa kipindi cha Desemba ambapo Simba na Yanga walikuwa katika ushiriki wao katika michuano ya kimataifa.
Kwa mujibu wa ratiba mpya kutoka Bodi ya Ligi Tanzania, mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Yanga yenyewe inatarajia kushuka dimbani Januari 30 kucheza dhidi ya timu ya Hausing FC ambayo inashiriki Ligi ya Mkoa wa Njombe.
Mechi hiyo namba 56, inatarajia kuchezwa saa 1 usiku katika Uwanja wa Azam Complex.
Huu utakuwa ni mchezo wa kwanza kwa Yanga kucheza ndani ya Tanzania Bara tangu mwaka huu uanze, mchezo wa mwisho kucheza ilikuwa ni ligi kuu ambapo walibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Tabora United kabla ya kwenda Zanzibar kushiriki michuano ya Mapinduzi Cup.
Mchezo namba 57, pia utachezwa siku hiyo mkoani Morogoro katika Uwanja wa Manungu, ambapo Mtibwa Sugar watawaalika Nyakagwe FC ya mkoani Geita.
Mara baada ya michezo, mwezi utafungwa kwa kushuhudiwa mechi nyingine mbili ambapo Simba SC, wao watashuka dimbani Januari 31, kucheza dhidi ya Tembo ya mkoani Tabora.
Mchezo huo hadi sasa bado haujapangiwa uwanja kutokana na uwanja waliokuwa wanatumia Simba, wa Uhuru kufungiwa na wenyeji walikuwa bado hawajatangaza uwanja mpya hadi sasa.
Mchezo wa mwisho wa funga dimba utakuwa ni kati ya Kagera Sugar ya mkoani Kagera ambao wakiwa katika uwanja wao wa Kaitaba watawaalika, Dar City ya Dar es Salaam.