Simba SC yatua Ivory Coast na kuanza kuiwinda Asec Mimosa

Wachezaji wa Simba SC, wakiwa mazoezini

KANDANDA Simba SC yatua Ivory Coast na kuanza kuiwinda Asec Mimosa

Na Zahoro Juma • 20:53 - 21.02.2024

Timu hizo zitaumana Ijumaa katika mechi za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika

Mara baada ya kufika tu nchini Ivory Coast, kikosi cha timu ya Simba SC chini ya Kocha, Abdelhak Benchikha, kimeingia moja kwa moja kwenye maandalizi kwa ajili ya mchezo wa Ijumaa wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji wao Asec Mimosa.

Akizungumza na Pulsesports akiwa nchini Ivory Coast, Mratibu wa Simba, Abbas Ally ambaye, ametangulia mapema kabla hata ya timu kufika, amesema hali ya hewa ya nchini humo haina tofauti na Tanzania, hivyo wachezaji wanatarajia kuwa katika hali za kawaida.

"Timu ilifika salama na tukapata muda wa kupumzika kabla ya kuanza maandalizi yetu siku ya leo na siku ya kesho tunatarajia kufanya mazoezi yetu ya mwisho katika Uwanja wa Stade Félix Houphouët Boigny ambao tutautumia kwa mechi ya Ijumaa,” amesema.

Asec ni vinara wa Kundi B wakiwa na alama 10 na tayari wamejihakikisha kufuzu hatua ya robo fainali tofauti na Simba ambao wapo nafasi ya pili wakiwa na alama zao 5.

Nafasi ya Simba kuungana na Asec inategemea zaidi mchezo huo wa kesho na ule wa mwisho ambao wataucheza katika Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es salaam, Machi Mosi dhidi ya Jwaneng Galaxy.

Katika mechi ya kwanza, waliocheza wakiwa Dar es Salaam, Simba walibanwa mbavu kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Asec.

Hata hivyo kuelekea mechi hiyo, Asec wanasaka rekodi ya kutokubali kufungwa kwenye mechi za hatua ya makundi hadi sasa lakini pia wanajua kuwa wana nafasi ya kuongoza kundi kwa kupata alama.

Tags: