Simba SC yatwaa Tuzo ya Mashabiki Bora wa AFL

KANDANDA Simba SC yatwaa Tuzo ya Mashabiki Bora wa AFL

Zahoro Mlanzi • 11:45 - 13.11.2023

Ilikuwa ni miongoni mwa timu nane ambazo zilishiriki michuano hiyo iliyofanyika kwa mara ya kwanza Afrika na uzinduzi wake ulifana katika ardhi ya Tanzania.

Baada ya Klabu ya Simba, kutwaa tuzo ya mashabiki bora katika michuano ya AFL, uongozi wa klabu hiyo, imesema ni heshima kubwa kwao kutwaa.

Simba SC ilikuwa ni miongoni mwa timu nane ambazo zilishiriki michuano hiyo iliyofanyika kwa mara ya kwanza na uzinduzi wake ulifana katika ardhi ya Tanzania na ndio sababu kubwa ya kutwaa tuzo hiyo.

Hata hivyo, Simba iliishia hatua ya robo fainali kwa kuondolewa na Al Ahly ya Misri.

Baada ya kutwaa tuzo hiyo, uongozi huo umesema ni ya kila shabiki wa Simba.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Salim Muhene 'Try Again', ndiye ambaye amekabidhiwa tuzo hiyo uwanjani Loftus Versfeld, Afrika Kusini baada ya kumalizika kwa fainali ya AFL ambapo Mamelodi Sundown ilitwaa ubingwa kwa kuifunga Wydad Casablanca kwa jumla ya mabao 3-2.

Try Again amesema: “Tuzo hii ni kwa kila shabiki wa Simba. Kuja kwenu uwanjani kushangilia timu yenu kumeiwezesha timu yetu kushinda Tuzo ya Mashabiki Bora wa AFL. Pongezi nyingi kwenu,”

Pia kwa upande wa Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema jambo hilo ni kubwa na linaleta heshima.

"Jambo hili ni kubwa kwetu, kama tumeanza kutambulika kwa upande wa mashabiki sasa tunajitafuta katika kuwa bora zaidi kwa timu, ni kitu ambacho kinawezekana," amesema.

Ameongeza timu yao imeanza kambi leo asubuhi kwa wale wachezaji ambao hawapo katika timu za Taifa kujiandaa na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Tags: