Simba yazindua jezi mpya kucheza na Al Ahly

© Kwa Hisani

KANDANDA Simba yazindua jezi mpya kucheza na Al Ahly

Zahoro Mlanzi • 10:00 - 13.10.2023

Michuano hiyo itazinduliwa kwa mara ya kwanza Oktoba 20, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo miamba hiyo itakuwa uwanjani kuumana kabla ya marudiano Oktoba 24.

Kikosi cha timu ya Simba, kimeingia kambini kujiandaa na michuano ya African Football League (AFL) dhidi ya Al Ahly ya Misri huku leo ikizindua jezi maalum kwa ajili ya michuano hiyo.

Michuano hiyo itazinduliwa kwa mara ya kwanza Oktoba 20, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo miamba hiyo itakuwa uwanjani kuumana kabla ya marudiano Oktoba 24.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa timu hiyo, Salim Abdallah 'Try Again', amesema jezi hizo zitaanza kupatikana katika maduka mbalimbali nchini.

"Tunaamini mwaka huu Wanasimba wameridhika na hata tukipita mtaani tunaona namna wamependeza na jezi zetu. Hongera Sandaland." amesema.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu, ameongeza: "Tupo imara, kila Mwanasimba atekeleze majukumu ili tufikie malengo yetu na kufikia hatua nzuri. Sandaland amekuwa mfano mzuri wa kazi anayofanya, Mdhamini Mkuu M-Bet, kampuni zote za Mo na wadhamini wengine wote."

Hata hivyo, Kipa namba moja wa timu hiyo, Aishi Manula ambaye amekuwa nje tangu Aprili, mwaka jana na beki Mkongo, Henock Inonga ‘Varane’ ambaye yupo nje kwa wiki mbili, sasa wako fiti na wameanza mazoezi.

Mchezaji majeruhi pekee aliyebaki Simba SC ni kiungo Muivory Coast, Aubin Kramo ambaye Madaktari wataendelea kumuangalia ili kujua anaendeleaje.

Katika hatua nyingine, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Temeke, Abdallah Mtinika, akizungumzia michuano hiyo, amesema:“Tutashirikiana vizuri sana na Klabu ya Simba”.

Amesema wana-Temeke ni watu wenye ushirikiano na wanapenda michezo na kwamba wapo tayari kupokea wageni na kuwaonesha fursa zilizopo Temeke na mambo mengine ya kimaendeleo na uwekezaji.

Tags: