Wajue makocha wanaopewa nafasi kuinoa Simba

KANDANDA Wajue makocha wanaopewa nafasi kuinoa Simba

Zahoro Mlanzi • 21:30 - 13.11.2023

Simba waliachana kwa amani na Robertinho siku chache tu baada ya kupokea kipigo kizito cha mabao 5-1 kutoka kwa Yanga kwenye mchezo wa Ligi Kuu uliofanyika Novemba 5.

Makocha watatu kutoka mataifa tofauti, wanatajwa huenda wakarithi mikoba iliyoachwa na Kocha, Mbrazil Roberto Oliviera 'Robertinho, aliyetimuliwa wiki iliyopita ndani ya Klabu ya Simba.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo, iliweka wazi kuwa mchakato wa kuziba nafasi ya Robertinho umeanza mara moja.

Simba imeingia katika wiki ya mapumziko kupisha mechi za timu ya taifa huku wakitoka kupoteza alama nyumbani walipotoka sare ya 1-1 na Namungo.

Akisisitiza hilo, Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema uongozi una lifanyia kazi suala la kocha mpya ndani ya kipindi hiki na kwamba mechi zitakapoanza tena watakuwa na kocha mpya.

Simba wanatarajiwa kuanza kampeni zao za hatua ya makundi wakiwa nyumbani wakicheza na Asec Mimosa na kisha watasafiri kuwafuata Jwaneng Galaxy ya Botaswana.

Wafuatao ni makocha wanaopigiwa chapuo kuvaa viatu vya Robertinho;

Sven Vandenbroeck

Taarifa nyingi zimekuwa zikimuhusisha Mbeligiji huyo ambaye alishawahi kuinoa Simba.

Aliwahi kupita Simba msimu wa 2019-20 ambao alichukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara na kisha msimu wa 20-21, baada ya kuisadia timu kufika hatua makundi aliondoka Januari, 2021 ambao alikwenda kujiunga na FAR Rabat ya Morocco.

Kwasasa hana timu baada ya kuachana na CR Beluizdad ya Algeria na kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali ni kwamba mwalimu huyo wapo kwenye mazungumzo na uongozi wa Simba na kama mambo yatakaa sawa basi atajiunga nao.

Julien Chevalier

Kocha wa viwango ambaye anakinoa kikosi cha Asec Mimosa ya Ivory Coast ambao pia ni wapinzani wa Simba katika hatua ya makundi ya Klabu Bingwa Afrika.

Kama unakumbuka vizuri msimu uliopita Simba walimchukuwa Robertinho kutoka Vipers ya Uganda huku timu hizo zikiwa zimepangwa kundi moja.

Msimu huu mshale bado unatembea lakini kati ya majina ambayo yanajadiliwa lipo jina la Chevalier ambaye ni raia wa Ufaransa.

Kocha huyo amedumu ndani ya Asec kwa msimu wa nne hadi sasa na ndiye alikuwa akiwafundisha kina Stephan Aziz Ki, Pacome Zouzoua, Kouassi Yao na Aubin Kramo.

Anapenda kufundisha soka la kuvutia lenye kasi na pia ni muumini mkubwa vijana wadogo.

Nasredine Nabi

Moja kati ya majina yanayoshtua kwenye orodha hiyo ni jina la kocha wa zamani wa Yanga, Nasredene Nabi ambaye kwasasa anakifundisha kikosi cha FAR Rabat ya Morocco.

Nabi alipita Yanga kwa mafanikio makubwa kwa misimu miwili mfululizo na kisha kuondoka msimu huu baada ya kuifikisha timu hiyo kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Jina la Nabi likitajwa isikusumbue kwani kabla ya kujiunga na Yanga tayari mafaili yake yalishafika kwenye meza za mabosi wa Simba kipindi hicho kocha huyo alikuwa anakinoa kikosi cha El Merreikh ya Sudan.

Hata hivyo, Simba walibadili gia angani wakamchukua Didier Gomez ambaye alitoka katika timu ya Al Hilal kwa kipindi hicho.

Kwahiyo jina la Nabi kurudi tena kwenye meza ya viongozi wa Simba sio jambo gumu ingawa ugumu uliopo pengine ni kuvunja mkataba wa kocha huyo na FAR Rabat ambao kwasasa ndio vinara wa Ligi ya Morocco.

Tags: