Mabasi 50 ya mashabiki wa Yanga yanakwenda Kigali kusapoti timu yao dhidi ya Al-Merreikh; mechi itachezwa Jumamosi uwanjani Pele.
Mabasi zaidi ya 50, yanaondoka saa 9 alfajiri ya leo kwenda jijini Kigali, Rwanda kwa ajili ya kutoa sapoti kwa timu yao ya Yanga itakayoumana na Al-Merreikh ya Sudan katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Timu hizo zitaumana Jumamosi kuanzia saa 10 jioni uwanjani Pele mjini Kigali ukiwa ni mchezo wa mkondo wa kwanza hatua ya kwanza ya michuano hiyo.
Ofisa Habari wa timu hiyo, Ally Kamwe, amesema kila kitu kimekwenda vizuri na mabasi 50 hadi sasa yamejaa tayari kwa ajili ya safari hiyo.
"Nashukuru kwa niaba ya Rais Injinia Hersi Said mashabiki na wanachama kwa mwitikio mzuri mliofanya...hadi sasa mabasi 50 kutoka mikoa mbalimbali yapo tayari kwa ajili ya safari ya kwenda Kigali," amesema Kamwe na kuongeza;
"Safari itaanza leo saa 9 alfajiri, msafara utaanzia makao makuu ya klabu, hivyo wale wanaosafiri tunaomba wazingatie muda na wahakikishe wanakuwa na hati ya kusafiria 'passport".
Katika hatua nyingine, Kocha wa Yanga SC, Miguel Gamond, amewashukuru watu wote waliohusika katika kuhakikisha timu hiyo inapata matokeo mazuri mwezi uliopita na yeye kuchaguliwa kuwa Kocha Bora wa mwezi.
Miongoni mwa watu aliowataja ni wachezaji wa timu hiyo, wafanyakazi waliopo ndani ya kambi yao Avic Town, wanaohudumia uwanja na benchi la ufundi.
“Muhimu zaidi ni wachezaji kwasababu sisi kama makocha sio chochote bila wachezaji”, amesema Gamondi kupitia video fupi iliyowekwa kwenye ukurasa rasmi wa Instagram wa timu hiyo.