Yanga SC matumaini kibao ikiifuata CR Belouizdad

KANDANDA Yanga SC matumaini kibao ikiifuata CR Belouizdad

Na Zahoro Mlanzi • 17:13 - 21.11.2023

Timu hiyo imeondoka nchini Tanzania ikiwa na wachezaji ambao hawakuitwa katika timu za Taifa

Timu ya soka ya Yanga SC, imeondoka nchini kwenda kukabiliana na CR Belouizdad ya Algeria katika mechi za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kikosi hicho kimeondoka nchini na wachezaji ambao hawakuitwa katika timu zao za taifa.

Mara baada ya wachezaji wengine kumaliza majukumu yao wataungana na timu huko Algeria.

Wachezaji wa Yanga ambao walikuwa na timu ya Taifa ya 'Taifa Stars' ni Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Ibrahim Abdullah 'Bacca', Metacha Mnata, Abutwalib Msheri, Nickson Kibabage na Mudathir Yahaya wao wataondoka kesho baada ya kumaliza mechi ya Morocco.

Kwa upande wa Stephan Aziz Ki, Khalid Aucho na Djigui Diarra wao wataunganisha kwenda Algeria baada ya kumaliza majukumu yao.

Yanga inatarajia kushuka uwanjani Ijumaa katika mchezo huo wa kwanza wa Kundi D, timu zingine zilizopo kundi moja na Yanga ni Al Ahly ya Misri na Medeama FC ya Ghana.

Mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa mgumu na muhimu kwa pande zote utaonesha taswira ya ushiriki wa Yanga katika hatua hiyo ikiwa ni mara ya kwanza baada ya miaka 25.

Akizungumzia safari ya Algeria, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa timu hiyo, Ally Kamwe, amesema katika uwanja wa mazoezi timu imeandaliwa vizuri na kwamba wanatarajia kwenda kuanza vizuri ili kuweka hai matumaini ya kufika mbali msimu huu.

Kamwe amesema wachezaji wote waliobaki kambini wapo fiti na kwamba wanatarajia makubwa.

Ameongeza wanajua kuwa mchezo wa ugenini hasa kwa timu kutoka Kaskazini mwa Afrika sio mwepesi lakini wao wanahitaji kufanya vizuri.

Tags: