Winga huyo ameachwa ili kutoa nafasi kwa winga mwingine Mghana, Augustine Okrah kupata nafasi ndani ya timu hiyo
Klabu ya Yanga, imetangaza kuachana na winga wake raia wa DR Congo, Jesus Moloko aliyedumu kikosini hapo kwa kipindi cha misimu miwili na nusu.
Moloko alijiunga na Yanga mwanzoni mwa msimu wa 2021-22 akitokea Klabu ya AS Vita ya nchini kwao na amefanikiwa kushinda mataji mawili ya Ligi Kuu Tanzania Bara, FA na Ngao ya Jamii.
Akiwa na kikosi hicho msimu uliopita, Moloko alikuwa sehemu ya kikosi cha kwanza cha Kocha Nasredein Nabi ambacho kilifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kufungwa na USM Alger.
Kuondoka kwa Moloko kwenye kikosi cha Yanga kunatoa nafasi kwa winga raia wa Ghana, Augustine Okrah kuchukuwa nafasi mara baada ya kusajiliwa mapema kwenye dirisha hili la usajili.
Dirisha la usajili kwa klabu za ligi kuu ambalo lilifunguliwa Desemba 15 litafungwa usiku wa leo.
Yanga katika dirisha hili mbali ya kumsajili Okrah lakini pia walimuongeza kikosini kiungo Shekhan Ibrahim kutoka JKU ya Zanzibar.
Pia mshambuliaji Crispin Ngushi alitolewa kwa mkopo kuelekea Coastal Union ya Tanga na tetesi zilikuwa zinaeleza kuwa mshambuliaji mwengine raia wa Ghana, Hafiz Konkoni huenda angetolewa kwa mkopo ili kupisha nafasi ya mshambuliaji mpya ambaye angetangazwa usiku huu kabla ya dirisha kufungwa.