Kama ombi lao litakubaliwa, Yanga itaanza kujipima na Dar City ya Ligi Daraja la Kwanza
Uongozi wa timu ya Yanga SC, umeweka wazi mipango yao ya maandalizi kuelekea michuano mbalimbali inayotarajiwa kurejea hivi karibuni.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, amesema kuanzia wiki ijayo Yanga watacheza michezo ya kimataifa ya kirafiki na ratiba wataiweka wazi kwa mashabiki na wanachama.
Amesema hiyo ni sehemu tu ya maandalizi ya kikosi chao ambacho kilianza mazoezi tangu mwanzo wa wiki iliyopita.
Moja ya mechi ambayo Yanga itaanza nayo kujifua ni dhidi ya timu ya Dar City.
"Kikosi kipo kwenye mazoezi makali na hadi kufikia mwanzo wa wiki ijayo wachezaji wote watakuwa kambini kasoro wale ambao wapo kwenye timu za taifa, tutaweka wazi ratiba za michezo ya kirafiki ili mashabiki waweze kuiona timu yao," amesema.
Ameongeza kwa kusema michezo hiyo inaweza kuwa ndani au nje ya nchi hivyo watu wajiandae kwa ajili ya kupata furaha na timu yao.
Yanga chini ya kocha, Miguel Gamondi, wameingia kambini mara tu baada ya kumaliza mapumziko yao waliyopata baada ya kushiriki michuano ya Mapinduzi Cup.
Baadhi ya nyota ambao wapo kambini wakiendelea na mazoezi ni Augustine Okrah ambaye alisajiliwa kwenye dirisha dogo la usajili na kisha akapata majeraha wakati akishiriki michuano ya Mapinduzi Cup.