Yanga SC yafunguka kichapo na Ihefu FC

© Kwa Hisani

KANDANDA Yanga SC yafunguka kichapo na Ihefu FC

Zahoro Mlanzi • 21:00 - 05.10.2023

Yanga imewatoa hofu mashabiki baada ya kipigo kutoka Ihefu FC, ikisema bado kuna mechi nyingi za kucheza na matumaini ni makubwa.

Klabu ya Yanga, imewatoa hofu wanachama na mashabiki wao kuwa ligi bado ndefu hivyo wana nafasi ya kufanya vizuri mechi zinazofuata.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara, juzi ilikumbana na kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Ihefu FC katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Highland Estate mjini Ubaruku, Mbeya.

Hicho ni kipigo cha pili mfululizo kwa Yanga, ikienda kucheza na timu hiyo kwenye uwanja huo huo.

Meneja Habari na Mawasiliano wa timu hiyo, Ally Kamwe, akizungumza na Pulsesports baada ya kurejea Dar es Salaam ikitokea Mbeya, amesema ndio kwanza wamecheza mechi nne ila bado kuna mechi 30 za kucheza zaidi hivyo mashabiki wasiwe na hofu.

“Ni sehemu ya matokeo ambayo yanapatikana kwenye ligi hivyo mashabiki wasikate tamaa wazidi kuwa pamoja na sisi kwa kuwa kuna mechi za kucheza na tunaamini tutapata matokeo chanya”.

Timu hiyo kwa sasa inajiandaa na mchezo mwingine dhidi ya Geita Gold utakaopigwa Jumamosi Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Katika hatua nyingine, Kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi, amesema wamepoteza mchezo kutokana na kufanya makosa na kupewa adhabu.

"Tuliwapa zawadi bao la kwanza kwani niliwaambia uwanja sio rafiki hakuna sababu ya kuazisha mashambulizi nyuma, wakafanya hivyo tukaadhibiwa, hakuna wa kumlaumu zaidi yetu wenyewe."

Amefafanua zaidi kupoteza mchezo huo si kutokana na kubadili kikosi ila makosa waliyofanya ndio yamesababisha kufungwa mabao hayo.

"Nikishinda natajwa kuwa kocha bora ila nikifanya mabadiliko katika kikosi na nikapoteza naanza kuhojiwa kwanini kocha amefanya mabadiliko, ndio mpira ulivyo, tumepoteza mchezo huo kwa bahati mbaya," ameongeza.

Tags: