Mafanikio hayo yametokana na kushinda ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania, ubingwa wa FA Cup na kufika hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Shirika la Kimataifa la Historia na Takwimu za Soka (IFFHS), limeitaja Klabu ya Yanga, kushika nafasi ya nne katika ubora wa viwango kwa Afrika ikitanguliwa na Al Ahly, Wydad Casablanca na Pyramids.
Orodha hiyo inaeleza wazi kuwa viwango hivyo ni kuanzia Novemba Mosi, 2022 hadi Oktoba 31, 2023.
Katika kipindi hicho, Yanga wamejipatia mafanikio mbalimbali ikiwemo kushinda ubingwa wa Ligi Kuu, ubingwa wa FA na kufika hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Yanga wanashika nafasi hiyo kwa kuvuna jumla ya alama 141 huku Al Ahly ambaye ndio kinara wa ubora akiwa na alama 244.
Wydad imeshika nafasi ya pili ikiwa na alama 153 kutokana na msimu uliopita kucheza fainali ya Klabu Bingwa Afrika lakini walipoteza taji mbele ya Al Ahly.
Mabingwa wa michuano mipya ya AFL, Mamelod Sundowns wao wapo kwenye nafasi ya tano nyuma ya Yanga wakiwa na alama 127.
Kwa upande wa watani zao wa jadi, timu ya Simba SC, wao wana alama 91 na wamejikuta wakishika nafasi ya 13 katika viwango hivyo ndani ya kipindi hicho kilichotajwa.
Klabu ya Manchester City ya Uingereza, yenyewe inaongoza kwa ubora duniani ikifuatiwa na Real Madrid huku Al Ahly wakiwa nafasi ya tatu.
Yanga wao kwa duniani wanashika nafasi ya 60 huku Simba wakiwa nafasi ya 148.
IFFHS ni Shirika linaloaminika kwa kukusanya takwimu mbambali za michezo duniani.
Moja kati ya takwimu zao ambazo zinatumika hadi leo nchini Tanzania ni kuhusu ubora wa Ligi ya Tanzania ambapo IFFHS waliitaja kuwa ya Tano Afrika.