Timu kubwa za Tanzania zimeungana kuisapoti Singida Fountain Gate dhidi ya Future FC ya Misri katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida miamba ya soka la Tanzania Bara, timu za Yanga SC, Simba SC na Azam FC, kwa mara ya kwanza zimeungana kuipa sapoti Singida Foutain Gate, katika mchezo wao wa Jumapili wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Future FC ya Misri.
Mchezo huo unatarajiwa kuanza saa 10 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Muungano huo unafanyika kwa mara ya kwanza katika karne ya 21, kwani timu hizo zimekuwa mahasimu wakubwa si katika michuano ya ndani hata ile ya kimataifa.
Ofisa Habari wa timu ya Singida FG, Hussein Massanza, amesema wameamua kuomba sapoti kwa timu hizo kubwa kutokana na mchezo huo kwao kuuchukulia kama wa kitaifa kutokana na umuhimu wake na ndio maana wameufanya uwe bure bila kiingilio.
"Tumeamua katika mchezo huu kwakuwa tunataka sapoti kubwa bila kujali itikadi zao na ndio maana Yanga, Simba na Azam kwa pamoja tumewaomba watuunge mkono katika mchezo huu kuwahawasisha mashabiki na wanachama wao kuwa kitu kimoja siku hiyo watushangilie," amesema Massanza.
Amesema kila mmoja aje na jezi yake siku hiyo ya mchezo na hata wasipovaa jezi wataingia tu uwanjani hakuna shida kikubwa wanataka kuona uwanja ukijaa na wanatoa sapoti.
"Hii ni mechi ya watanzania wote na ni ya kitaifa na kutokana na ukubwa wa mchezo huu, tumeaandaa jezi maalum kwa viongozi wa kitaifa kuanzia kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wake, Dkt. Philip Mpango, Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Naibu Waziri Mkuu, Doto Biteko, kama watapata nafasi waje uwanjani wakiwa na jezi zao kushuhudia mchezo," amesema Massanza.
Amewaomba mashabiki watakaokuja uwanjani kuweka ushabiki pembeni na kuisapoti timu yao ili wageni wajione kweli wapo ugenini.
Kwa upande wa Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Yanga, Ally Kamwe, amesema kwakuwa ni mechi ya kimataifa ndio maana wameamua kusapoti mchezo huo kwa manufaa ya taifa.
"Nimekuja hapa kwa ajili ya mambo ya Kitanzania, tutabishana na kutambiana katika masuala ya ligi yetu lakini linapokuja suala la utaifa tunakuwa kitu kimoja, hivyo mashabiki wa Yanga kwa umoja wetu mjitokeze kwa wingi kuisapoti Singida FG," amesema Kamwe.
Pia Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa timu ya Azam FC, Thabit Zakaria 'Zaka Zakazi', amesema licha ya timu yao kutolewa mapema katika michuano ya kimataifa, wataungana na Singida FG kuhakikisha wanaipeperusha vizuri Bendera ya Taifa.
Meneja Mawasiliano wa timu Simba, Ahmed Ally, amesema ni jukumu lao kusaidia timu zingine ziwe zinafanya vizuri kimataifa kama ambavyo wao wamekuwa wakifanya katika misimu mbalimbali.