Ushindi huo, unaifanya Yanga kulipa kisasi cha miaka 10 iliyopita kwani mwaka 2013 nao walifungwa mabao 5-0 na Simba
Ni gharika! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya timu ya Yanga SC, kuibuka na ushindi wa mabao 5-1 mbele ya watani zao wa jadi, Simba SC katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Ushindi huo, unaifanya Yanga kulipa kisasi cha miaka 10 iliyopita kwani mwaka 2013 nao walifungwa mabao 5-0 na Simba.
Mabao ya Yanga katika mchezo huo uliopigwa mbele ya maelfu ya mashabiki wa soka Tanzania, yalifungwa na Kennedy Musonda, Max Nzengeli aliyefunga mawili, Stephane Azizi KI na Pacome Zouazoa kwa mkwaju wa penalti.
Bao pekee la Simba, lilifungwa na Kibu Denis ambaye hata hivyo hakumaliza mchezo kutokana na kupata majeraha ya kifundo cha mguu na kutolewa nje.
Ushindi huo, umeifanya Yanga, kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo kwa kufikisha alama 21 huku Simba ikiwa nafasi ya tatu kwa alama `18 na Azam inashika nafasi ya pili kwa alama 19.
Hata hivyo, Simba ipo nyuma kwa mchezo mmoja.
Mechi hiyo ilitawaliwa na hofu hasa kutokana na mvua kubwa iliyoendelea kunyesha katika jiji hilo kwa takribani siku tatu mfululizo, ikidhaniwa huenda mchezo huo usifanyike kama mvua ingeendelea kunyesha.
Yanga ndio ilikuwa ya kwanza kufunga bao la mapema katika dakika ya tatu likifungwa na Musonda kwa kichwa akiunganisha krosi ya Kouassi Attoula Yao ikiwa ni asisti yake ya tano katika ligi hiyo.
Bao hilo halikudumu muda mrefu kwani dakika ya 8, mshambuliaji Kibu, aliisawazishia timu yake ya Simba, akifunga kwa kichwa akiunganisha kona ilichongwa na Saido Ntibanzokiza.
Baada ya kuingia kwa mabao hayo kulifanya mechi kuamka zaidi na kila timu kuonekana kujipanga kwa ajili ya kutafuta bao la pili.
Hata hivyo, hadi Mwamuzi, Ahmed Arajiga anapuliza kipyenga cha mapumziko timu hizo zilikuwa sare ya 1-1.
Kipindi cha kwanza mlinzi wa Yanga, Dickson Job na kiungo wa Simba, Fabrice Ngoma walioneshwa kadi za njano kwa nyakati tofauti kutokana na mchezo usiokuwa wa kiungwana.
Katika kipindi cha pilia ambacho Simba ilionekana kufunguka zaidi bila kuwa na tahadhari ya kuzuia ndipo Nzengeli alipofungua karamu ya mabao kwa kufunga bao la pili akiitendea haki pasi ya Aziz KI.
Kama hiyo haitosha, Aziz KI ambaye alikuwa na mchezo mzuri alifunga bao lake la saba msimu huu na la tatu katika mchezo huo baada ya kupokea pasi kutoka kwa Clement Mzize aliyeingia kipindi cha pili kuchukuwa nafasi ya Musonda.
Karama ya mabao kwa Yanga haikuishia hapo kwani Nzengeli kwa mara nyingine tena alifunga bao la nne, akitumia pasi ya Mzize wakiwa ndani ya eneo la hatari na hilo likiwa ni bao lake la saba msimu huu akiwa sawa na KI.
Nzengeli ambaye kwa kiasi kikubwa kipindi cha kwanza hakuonekana uwanjani alisababisha penalti baada ya kufanyiwa madhambi na mlinzi, Henock Inonga na mpira huo kukwamishwa wavuni na Pacome Zouzoua ambaye naye alikuwa na kiwango bora.