Yanga yatua Dar na faili la Al Ahly

KANDANDA Yanga yatua Dar na faili la Al Ahly

Na Zahoro Mlanzi • 18:00 - 26.11.2023

Timu hiyo itashuka uwanjani Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kuumana na miamba hiyo ya soka la Misri na Afrika kwa ujumla

Timu ya Yanga SC, imetua nchini Tanzania salama ikitokea Algeria na kuahidi kufanya vizuri katika mchezo wao ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly kutokana na kuijua vizuri timu hiyo.

Pia timu hiyo imetoa mapumziko ya siku kadhaa kabla ya Jumanne kuingia rasmi kambini kujiandaa na mchezo huo.

Mchezo huo unatarajiwa kupigwa Jumamosi Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam ambapo Yanga wataingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya kipigo cha 3-0 kutoka kwa CR Belouizdad katika mchezo uliuofanyika Ijumaa.

Akizungumza na Pulsesports baada ya kutua nchini Tanzania, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, amesema wametoa mapumziko mafupi kwa wachezaji kabla ya kukusanyika Jumanne kwa ajili ya kuanza maandalizi.

Amesema wamepoteza mchezo wa kwanza ambao kulikuwa na haja kubwa ya kufanya vizuri lakini bahati mbaya matokeo hayakuja kwa upande wao hivyo katika mchezo wao wa nyumbani watahakikisha wanarekebisha makosa.

"Sisi tunakwenda kwa hesabu, tulitaka kufanya vizuri ugenini lakini imeshindikana, mechi hiyo imeshapita sasa tunaangalia mechi yetu muhimu ya nyumbani dhidi ya Al Ahly," amesema.

Amesisitiza mashindano ndio kwanza yanaanza na kwamba bado kuna alama nyingi za kutafuta tofauti na zile walizopoteza katika mchezo wa kwanza.

Kuhusu hali ya kikosi Kamwe, amesema wachezaji wote walimaliza mchezo wakiwa katika hali nzuri na wanatarajia kuwa pamoja katika maandalizi ya mchezo huo wa Jumamosi.

Alisema kukosekana kwa kipa namba moja, Djigui Diarra katika mchezo dhidi ya CR Belouizdad, haikutokana na majeraha bali ni kuchelewa kuripoti kambini nchini Morocco wakati akitoka katika timu yake ya Taifa ya Mali.

Al Ahly ndio mabingwa watetezi wa michuano hiyo na wana alama 3 sawa na CR katika Kundi D baada ya kuifunga Medeama ya Ghana kwa mabao 3-0.

Tags: